FACEBOOK

LightBlog

Breaking

LightBlog

Friday 28 November 2014

Sababu ya kufunguliwa akaunti ya escrow.

.
zittoMwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ameanika chanzo cha kufunguliwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow kuwa ni mgogoro ulioibuka kati ya Tanesco na IPTL.
Akitoa ripoti ya uchunguzi wa akaunti ambayo Sh306 bilioni zilichotwa na IPTL, Zitto alisema ilianzishwa chini ya wanahisa wawili; Kampuni ya Mechmar Malaysia Berhad iliyosajiliwa Malaysia ambayo ilikuwa inamiliki hisa saba sawa na asilimia 70 katika IPTL na Kampuni ya VIP Engineering and Marketing iliyosajiliwa nchini ikiwa na hisa tatu sawa na asilimia 30 ya hisa zote.
Alisema mwaka 1995, Serikali kupitia Tanesco iliingia Mkataba wa miaka 20 na IPTL kwa ajili ya kuzalisha na kuuziana umeme wa megawati 100 japokuwa makubaliano ya awali (MoU) yalionyesha kuwa mkataba ungekuwa wa miaka 15.Kusoma zaidi bofya
“Hata hivyo, Tanesco ilibaini kwamba gharama za ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme ambazo IPTL iliwasilisha kwake zilikuwa kubwa tofauti na makubaliano ya kwenye mkataba,” alisema. Alisema IPTL ilikuwa imefunga injini zenye msukumo wa kati (medium speed) zenye gharama ndogo na uwezo mdogo badala ya injini za msukumo mdogo (low speed) zenye nguvu kubwa na bei kubwa.
“Wakati huohuo, IPTL waliendelea kutoza kiasi kikubwa cha fedha kinacholingana na gharama ya ufungaji wa mtambo wenye msukumo mdogo (low speed). Katika utekelezaji wa Mkataba IPTL walitakiwa kufunga jenereta tano zenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 kila moja lakini badala yake walifunga jenereta 10 zenye uwezo wa kuzalisha megawati 10 kila moja, jambo ambalo lilikuwa ni kinyume na makubaliano ya mkataba,” alisema.
Kutokana na IPTL kukiuka mkataba, alisema mwaka 1998 Tanesco ilifungua kesi katika Baraza la Kimataifa la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kupinga ukiukwaji huo na hukumu iliyotolewa na ICSID; IPTL iliagizwa kupunguza gharama za uwekezaji kutoka Dola 163.531 milioni hadi 127.201 milioni kwa mwezi. Alisema ujenzi wa mitambo ulikamilika mwaka 1997, uzalishaji na uuzaji wa umeme ulianza mwaka 2002.
Alisema kuanzia mwaka 2002, gharama za uwekezaji kutokana na uwepo wa mtambo wa kuzalisha umeme, zilianza kulipwa na Tanesco kwa IPTL, huku gharama za uendeshaji zikiendelea kulipwa kwa muda wote ambao mkataba unaendelea bila ya kujali kama mtambo unazalisha umeme au hauzalishi.
“Gharama zilikoma kulipwa moja kwa moja kwa IPTL mwaka 2007 baada ya Tanesco kubaini kuwa IPTL inakokotoa gharama hizo kwa msingi wa Dola 38.16 milioni (ambayo ni sehemu ya mkopo wa Dola 105 milioni uliochukuliwa na wanahisa kutoka umoja wa benki za Malaysia, ambao baadaye ulinunuliwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong, badala ya mtaji wa uwekezaji wa Sh50,000 uliosajiliwa Brela.)
“Hali hii ilifanya tozo ya gharama za uendeshaji kuwa kubwa. Endapo ungetumika mtaji wa uwekezaji wa Sh50,000 katika kukokotoa gharama za uendeshaji, Tanesco ingekuwa inalipa tozo ndogo kuliko ilivyo sasa,” alisema.
Alisema hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya mwaka 2004, Tanesco kufungua kesi ya pili kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya gharama za uendeshaji na kwamba uamuzi wa Baraza ilikuwa ni wanahisa waketi na mteja wao (Tanesco) na kukubaliana kuhusu kanuni ya ukokotoaji wa tozo hiyo.
“Mpaka sasa tunapowasilisha taarifa hii bungeni, uamuzi wa ICSID-2 kwamba IPTL ikae na Tanesco kwa ajili ya kukokotoa upya gharama za uendeshaji haujatekelezwa, hivyo Tanesco wanaendelea kulipa Dola za Marekani 2.6 milioni (Sh4.5 bilioni kwa mwezi),” alisema.
Escrow kufunguliwa
Zitto alisema kwa mujibu wa taarifa ya CAG, imebainika kuwa chanzo cha mgogoro kati ya Tanesco na IPTL ambacho ndicho kilichosababisha kufunguliwa kwa Akaunti ya Tegeta Escrow ni taarifa ziliyoifikia Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco.
Alisema katika taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine ilifahamishwa na mmoja wa wanahisa wa IPTL, Kampuni ya VIP Engineering, kuwa kuna viashiria kuwa Tanesco wanailipa IPTL gharama kubwa za uendeshaji.

No comments:

Adbox