Tukio hilo la kusikitisha lilitokea wiki iliyopita ambapo kwa mujibu wa ndugu wa marehemu na majirani, wanandoa hao walikuwa na ugomvi tangu Agosti mwaka huu ambapo mume alikuwa akimshutumu mkewe kwamba anachepuka njia kuu.
DADA WA MKE ASIMULIA
Akizungumzia mkasa kamili, dada wa marehemu Mery, mama Jane aliweka wazi mkasa mzima wa mauaji hayo akisema mwezi uliopita, shemeji yake huyo alifika nyumbani kwake na kumshtakia kwamba hawaelewani na mdogo wake ndani ya nyumba kutokana na kupigiwa simu mara kwa mara na wanaume hivyo amkanye.Akuzungumza na Uwazi huku akilia kwa uchungu kutokana na aina ya kifo cha mdogo wake, mama Jane alisema:
“Hivi karibuni, Isaya alikuja nyumbani, akaniambia Mery alipigiwa simu na mwanaume akatoka kwenda kupokelea nje, akamsikia akisema nipigie baadaye mume wangu yupo.“Alisema alipomuuliza mkewe kwamba ulikuwa unaongea na nani, alimjibu hayakuhusu, ndipo akachukua hatua ya kuja kwangu na kuniambia nizungumze naye,” alisema dada mtu huyo.
MDOGO MTU AONYWA
Mama Jane akaendelea kusema: “Nilikaa na mdogo wangu, nikaongea naye tukamaliza nilimwambia amsikilize mumewe, maana huu ni mji, lakini sikujua kilichoendelea kwa vile mimi nilisafiri kwenda nyumbani Tabora, nilirudi siku moja kabla ya tukio lakini sikuwa nimeonana na mdogo wangu.”
Mama Jane alisema kuwa, baada ya yeye kurudi kutoka Tabora siku iliyofuata alikwenda kwa mdogo wake kwenye sehemu aliyokuwa akifanyia biashara ya kukaanga mihogo lakini hakumkuta.
“Niliwauliza majirani, wakaniambia kwamba Mery alikwenda kuchukua mihogo Mbezi, nikaamua kurudi nyumbani kwangu na kuendelea na mambo mengine.
“Kesho yake asubuhi, nakumbuka ilikuwa Jumapili nilikwenda tena kwenye kibanda chake cha biashara pia sikumkuta, nikarudi kwangu lakini nikapanga mchana niende nyumbani kwake baada ya kumalizana na wageni waliofika nyumbani kwangu kunisalimia.”
NDUGU AMFUATA DADA, AMJULISHA KIFO
Mama Jane aliendelea kusema: “Lakini kabla sijamalizana na wageni alikuja kijana mmoja, ni mtoto wa kaka yangu akaniambia kwamba Mery amefariki dunia.
“Nilichanganyikiwa sana, nikatoka mbio kuelekea nyumbani kwa Mery huku nikiomba kwa Mungu isiwe kweli. Kufika nikakuta umati ukichungulia ndani kupitia dirishani maana mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani.“Nilitamani hali ile iwe ndoto. Nilisema moyoni kwamba huenda nitapata habari tofauti na zile za Mery kufariki dunia. Nilijiuliza Mery amekufaje? Mumewe je? Yuko wapi?”
ASHUHUDIA MWILI WA MAREHEMU KUPITIA DIRISHA
Mama Jane anaendela kusimulia: “Nilifanikiwa kuchungulia dirishani ambapo niliumia sana kwa kuushuhudia mwili wa mdogo wangu ukiwa umetapakaa damu huku ukiwa chali kitandani. Nikashtuka tena kumwona mumewe naye akiwa ananing’inia kwa kujinyonga chumbani humohumo.
“Nililia sana, niliishiwa nguvu zote, ndipo polisi waliitwa kuja kuvunja mlango ambapo waliibeba miili ya marehemu wote hadi hospitali kwa ajili ya uchunguzi.“Uchunguzi wa awali ulibaini kwamba, mdogo wangu alishindiliwa sululu ya kifuani ikaenda kutokea mgongoni na nyingine kwenye paji la uso ikatokea kisogoni, da! Inauma sana kwa kweli.
“Baadhi ya watu walisema alipomaliza kufanya hivyo wakati mdogo wangu ameshafariki dunia akachukuwa kamba na kujimalizia kwa kujinyonga.”
HISTORIA FUPI
Mama Jane aliizungumzia historia fupi ya ndoa ya mdogo wake na mumewe, Isaya, alisema:
“Mdogo wangu na huyo Isaya walianza kuishi kama mume na mke mwaka jana. Isaya alikwenda kumchukuwa nyumbani kwa wazazi Tabora na kuja naye hapa Dar.”
HUZUNI YATANDA
Waombolezaji waliohudhuria kwenye msiba huo walionekana kuwa na huzuni pia hofu ikitawala huku kila mmoja akizungumzia lake kuhusu tukio hilo.
MWILI WA MWANAMKE WASHINDWA KUFUNULIWA
Miili yote iliagwa Goba nyumbani kwa marehemu hao na kuzikwa katika Makaburi ya Kwarobert, Mbezi jijini Dar, Jumanne iliyopita.
No comments:
Post a Comment