Rais
Jakaya Kikwete amezungumzia nia ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, January Makamba kutaka kuwania urais mwakani, akisema
mwanasiasa huyo kijana “anataka mambo makubwa, lakini hajamshirikisha”.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kutoa maoni yake kuhusu wanachama wa
CCM wanaotaka kuwania urais, baada ya chama hicho kuwaonya makada sita
kwa tuhuma za kuanza mapema kampeni za kutaka nafasi hiyo kubwa.
Akiwa
jijini London, Makamba alitangaza nia yake ya kuwania urais mwaka 2015,
akisema huu ni wakati wa fikra mpya ambazo zinahitaji vijana na kwamba
wazee wakae kando.
Jana,
Rais Kikwete, ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika
Kata ya Soni Bumbuli mkoani Tanga anakoendelea na ziara ya siku tano,
alimtaka Makamba “asilazimishe” kwa kuwa wakati ukifika atapata kile
anachokitaka.
“Nasikia
kuwa bwana mdogo January anataka mambo makubwa. Mie hajaniambia, na mie
nasikia. Hata alipogombea ubunge hakuniambia nilisikia baadaye...
asilazimishe, wakati ukifika atapata, na akikosa asilete nongwa,”
alisema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete alitoa mfano wake mwenyewe aliposhindwa katika uteuzi wa
mgombea urais wa CCM mwaka 1995, wakati akiwa na miaka 45 (miaka minne
zaidi ya umri wa Makamba ifikapo 2015), akisema kuwa hakukata tamaa na
aliendelea kusikiliza ushauri wa wazee hadi alipofanikiwa kukalia nafasi
hiyo ya juu mwaka 2005.
Mwenyekiti
huyo wa CCM, ambaye pia ushawishi wake unaweza kuamua mteule wa chama,
alimtaka mbunge huyo wa Bumbuli asikilize ushauri wa wazee.
Pamoja
na ushauri huo kwa mwandishi wake wa zamani wa hotuba, Rais Kikwete
alimpongeza kwa kazi nzuri ya ubunge jimboni humo na akaeleza kuwa
anamsaidia katika wizara yake.
Alinukuu
maneno ya aliyekuwa katibu mkuu wa Afro Shiraz na swahiba wake, Thabit
Kombo aliyemwambia Kikwete kuwa “wakati ukifika utapata”, hasa kutokana
na kiu yake ya muda mrefu ya kuwatumikia Watanzania.
“Nilipokosa
mwaka 1995 sikukata tamaa, ndipo 2005 nikaingia, na huo ndio ulikuwa
wakati wangu wa kushika wadhifa huu. Wakati ukifika watu watake wasitake
utakuwa wewe tu,” alisema Kikwete.
Kauli
hiyo ya Rais Kikwete imekuja takriban wiki moja baada ya Makamba
kueleza nia yake ya kuwania urais akisema kwa asilimia 90 ameshaamua
kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Mbunge
huyo wa Bumbuli, ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf
Makamba, alitangaza uamuzi huo akiwa Uingereza alikokuwa akihudhuria
mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa na Shirika la
Utangazaji la Uingereza (BBC) na baadaye kufafanua nia hiyo katika
mahojiano na gazeti hili.
Rais
Kikwete akimshauri asikilize ushauri wa wazee, wakati akitangaza nia
hiyo Makamba alisema: “Ni wakati wa fikra mpya kushika dola na mimi
ninaona kwamba wazee wakae kando. Mfano awamu moja inapoondoka na wazee
walioko katika mfumo wakae kando ili kupisha fikra mpya kuongoza dola.”
alisema Makamba ambaye kwa sasa ana miaka 40.
Makamba
ameendelea kusisitiza nia yake hiyo na kutetea nafasi ya vijana katika
nafasi hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook akisema: “Tanzania mpya
inahitaji viongozi wapya, mazoea mapya, fikra mpya na maarifa mapya.
Inahitaji kuthubutu mambo makubwa siyo kulinda uzoefu wa nyuma.”
Makamba
ni mmoja wa makada sita wa CCM walioonywa na chama hicho mapema mwaka
huu kwa kutuhumiwa kuanza mapema kampeni za urais kinyume na utaratibu,
lakini chama hicho hakijaona kasoro katika uamuzi wake wa kutangaza nia.
CCM yambariki
Katika
hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimebariki mbio za Makamba
baada ya jana kueleza kuwa hajafanya kosa lolote kwa kutangaza nia yake.
Katibu
wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema alichofanya Makamba ni
tofauti na adhabu ambayo chama hicho kilimpa yeye na wenzake watano
miezi mitano iliyopita.
Nape
aliwataka wanaohoji suala hilo kurejea adhabu iliyotolewa na CCM,
Februari 18, mwaka huu kwa makada wake sita baada ya kukutwa na makosa
ya kuanza mapema kampeni za urais mwaka 2015, akiwamo Makamba.
Wengine
waliokutwa na rungu hilo ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na
Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu),
Stephen Wassira, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe na William
Ngeleja.
“Hili
jambo linakuzwa tu wakati katika barua tulizowapa tulieleza wazi.
Waambie wawaonyeshe barua ambazo chama kimewapa ili mjue nini ambacho
hawatakiwi kukifanya,”alisema Nape.
“Yeye
amesema akipewa ridhaa ya kugombea urais, jambo hili halipo kati ya
makosa ambayo yalisababisha yeye na wenzake kupewa adhabu.”
Februari
18, mwaka huu Kamati Kuu ya CCM ilitoa adhabu kwa makada hao baada ya
kuthibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya
wakati kinyume na kanuni za uongozi na uaadili za chama hicho.
Hata
hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula aliwahi kukemea tabia
ya baadhi ya wana-CCM kutangaza mapema nia ya kugombea nafasi mbalimbali
za uongozi katika uchaguzi ujao, akisema ni wasaliti wakubwa ndani ya
chama.
CCM
pia ilitoa mwongozo na kanuni za uchaguzi ambazo Ibara 6 (2) (1-5) ya
Maadili ya Viongozi wa CCM inawazuia wanachama kutoa michango, misaada,
zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya
kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la
Februari 2010, Ibara 6 (7)(i), ni kinyume kwa wanachama wake kutafuta
kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati.
via>>Mwananchi
No comments:
Post a Comment