MELANIA kamanda Janette anayetafutwa kwa mauaji ya halaiki ya watu
katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo baada ya kuvuka milima na mabonde
kwa kukwepa vikwazo vyote ambavyo kwa uwezo kibinadamu ni vigumu kuvuka
bali kwa nguvu za Mungu tu. Hatimaye kafika nchini Tanzania, dhamira
yake ya kutaka kuzungumza na waandishi wa habari ili kujua ana kitu gani
moyoni mwake inatimia. Anafanikiwa kuitisha mkutano na waandishi wa
habari wa vyombo vyote. Yupo mbele ya waandishi anataka kuwaambia nini?
Je, taarifa yake serikali ya Tanzania itaipokeaje?
SONGA NAYO...
WAANDISHI wote walikuwa makini kusikiliza kinachotaka kuzungumzwa na wanawake wawili waliokuwa mbele yao wakionekana wacha Mungu kutokana na mavazi ya kitawa. Janette alikohoa kidogo na kuanza kusema kwa sauti ya kati.
“Habari zenu ndugu waandishi wa habari kutoka vituo mbalimbali?”
“Nzuri,” waliitikia kwa pamoja.
“Kwanza napenda kuwashukuru wote mliofika hapa kwa kuacha kazi zenu kuja
kunisikiliza, nina imani siku ya leo ni muhimu niliyoitafuta kwa jasho
la damu na maji lakini namshukuru Mungu kaweza kunifikisha nyumbani
baada ya safari ndefu ambayo sitaisahau maishani mwangu.
Ndugu waandishi wa habari wa vyombo vyote ulimwenguni, nina imani
tuliokaa mbele yetu tunaonekana wacha Mungu tulioshiba imani ya
kumtambua Mungu. Pia mna shauku kujua tulichowaitia kwenye ukumbi wa
Hoteli ya Kempisky. Nia na madhumuni ni kusema mengi yaliyojaa moyoni
mwangu ambayo yameficha siri nzito.
“Najua mtashangaa kwa nini najinadi peke yangu japokuwa tupo wawili, ipo
sababu ya kufanya kwa vile asilimia tisini na tisa pointi tisa kikao
hiki kinanihusu mimi. Kwa jina naitwa Melania Johnson jina nililokaa
nalo kwa miaka mitatu tu na aliye pembeni yangu ni mama yangu mzazi
anaitwa anaitwa Lovenes Johnson.
“Kiumri ni msichana mdogo lakini maisha niliyopitia mpaka kufika hapa ni
zaidi ya mtu aliyeishi miaka elfu moja chini ya jua. Nia na madhumuni
ni kuwaeleza mkasa mzito ambao utautesa moyo wangu mpaka Mungu
atakapozichukua pumzi zangu.
“Historia yangu inaanzia toka muda mfupi siku tulipotoka nchi ya Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo nikiwa na baba yangu kipenzi kumtembelea mama
yangu kipenzi aliyekuwa huko akifanya kazi katika shirika la kimataifa
la kuhudumia wakimbizi( UNHCR).”
Baada ya kufika hapo alishindwa kuendelea kuongea na kuanza kulia kilio
cha kwikwi huku mama yake akimbembeleza kwa kumpigapiga mgongoni baada
ya kukumbuka kifo cha baba yake kilitokana na amri yake baada ya
kuwateka wanajeshi wa serikali wakiwemo wazazi wake bila kujua. Lakini
bila kujua aliamrisha wanajeshi wale wauawe akiwemo baba yake kipenzi .
Baada ya kufuta machozi na kamasi nyembamba aliendelea kuzungumza huku waandishi wakiwa wametulia kumsikiliza.
“Inauma kila nikikumbuka kifo cha marehemu baba yangu, ambaye naweza
kusema nahusika bila kujua kama nilikuwa nampoteza kipenzi changu.
Kutokana na maelezo ya mama siku hiyo ya mwanzo wa historia mbaya, hii
ilitokea alipotuaga uwanja wa ndege wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
na ndege tuliyopanda kupata ajali kwenye misitu ya Kongo muda mchache
baada ya kuondoka.”
“Inasemekana tulikuwa watu hamsini lakini tulipona wawili mimi na baba,
lakini nilipotezana na baba na mimi kuchukuliwa na kikundi cha waasi wa
Congolese Patriotic Front nikiwa na miaka mitatu tu. Nimekuja kukutana
na baba yangu baada ya miaka kumi na saba na kumfahamu akiwa marehemu.
“Inauma...inauma, namuomba huko alipo baba yangu anisamehe sikuwa na nia
ya kumuua ila mazingira yalifanya iwe hivyo. Nashukuru nilimzika baba
yangu kwa heshima zote tofauti na wanajeshi wengine wa serikali ambao
tuliwafukia shimo moja.
“Maisha yangu yote toka nikiwa na miaka mitatu sikulelewa na wazazi
wangu bali waasi. Hapo ndipo jina na Melania lilipokufa na kuzaliwa la
Janette,” jina lile liliwafanya watu wote washtuke huku usalama wa taifa
wakipeana taarifa ya kuwa kikazi zaidi kwani waliamini mtu aliyekuwa
pale anaweza kuwa yule Kamanda Janette anayetafutwa kwa muaji ya halaiki
ya watu katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo kutoka na maelezo
yake ya awali.
Janette aliendelea kuwaeleza maisha yate aliyoishi katika jeshi la
waasi, hakutaka kueleza kuwa cheo alichopewa cha kamanda ni chake bali
alielezea tu kuwa alishiriki katika mauaji wa watu wasio na hatia kwa
shinikizo la watu waliomlea.
“Kwa kweli kila nilichokifanya hakikuwa kwa hiyari yangu bali kwa
shinikizo na kulishwa roho mbaya na kukua nayo baada kukutana na hali
ile iliyonifanya niamini kabisa sisi ndiyo tulikuwa na haki ya kutawala
serikali ya DRC.
“Niliichukia serikali kwa kuamini walikuwa wakitumia mabavu kutawala lakini ipo siku na sisi tutaingia ikulu ya DRC huku nikiahidiwa nafasi ya juu serikalini. Naweza kusema sababu ya mimi kuonekana kamanda ilitokana kuwa na uhusiano wa kimapenzi na kamanda wa Kundi la Congolese Patriotic Front kwani baada ya kufa nilipewa cheo hicho.”
Janette aliendelea kuelezea jinsi alivyokutana na mama yake ambaye
anaamini ni Mungu ndiye aliyetaka akutane naye baada ya kuangalia picha
kwenye begi alilokuwa amebeba muda mfupi kabla risasi hazijachukua uhai
wake wakati huo tayari baba yake alikuwa ameishamiminiwa risasi.
Baada ya kugundua ni wazazi wake alichanganyikiwa na kutaka kumuokoa
baba yake ambaye wakati huo hali ilikuwa mbaya sana kutokana na kupoteza
damu nyingi kutokana na majeraha ya risasi. Lakini alijitahidi mpaka
pumzi za mwisho na baba yake kufia mikononi mwake.
“Kinachoniumiza ni jinsi wazazi wangu walivyonitafuta mtoto wao kwa
kujitoa maisha yao lakini bila kujua amri yangu inachukua mapenzi wa
baba yangu aliyekuwa akinitafuta mtoto wake wa pekee,” kufika hapo
Janette alianza kulia tena kwa uchungu kwa kukumbuka kifo cha baba yake
aliyejitoa mhanga kumtafuta mwanaye na yeye kuwa chanzo cha mauti yake.
Simulizi ya Janette iligusa moyo wa kila mwandishi aliyekuwepo ukumbini
na kujikuta akidondokwa na chozi kila Janette alipozungumza kwa hisia
kali na kilio cha uchungu.
“Nina imani ninatafutwa kila kona ya dunia taarifa zangu zipo kila
sehemu ili nikamatwe na kupelekwa katika mahakama ya kimataifa ya
uhalifu wa kivita (The Heague). Nipo tayari kushtakiwa kama dunia
itaniona nina makosa kwa vile naamini bila ajali ningekuwa na maisha ya
amani chini ya uangalizi wa wazazi wangu.
“Mwanzo sikujishangaa kuwa katika jeshi la waasi kwa vile niliamini
kabisa mimi ni Mkongomani mwenye haki ya kuishi ndani ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo pia kutawala kama wengine. Na yote yaliyofanyika
wakati ule niliamini ni sahihi kwa vile tulikuwa tukipigania nchi yetu.
“Lakini toka nilipokutana na mama yangu na kunieleza sababu ya mimi kuwa
kule, moyo wangu uligeuka mara moja na kumlilia Mungu kwa yote
niliyoyafanya. Ninaamini siku zote kuua ni jambo baya lakini kutenda
jambo bila kujua Mungu hawezi kukuhukumu bali kulitenda ukijua.
“Ningeweza kujisalimisha katika jeshi la Kongo lazima wangeniua kwa vile
mimi ndiye niliyeonekana adui yao namba moja hasa baada ya kuweza
kuiziba nafasi ya marehemu mpenzi wangu. Walinitafuta usiku na mchana
waniue, lakini Mungu alinilinda aliamini kuna siku nitajijua mimi ni
nani na kuachana na roho ya mauaji.
“Baada ya kujitambua ndipo nilipotoroka na kupata upinzani mkubwa toka
kwa wenzangu ambao hawakutaka niondoke waliniona msaliti. Kwa uweza wa
Mungu niliweza kuondoka kwenye kambi hiyo japo walifanikiwa kunipiga
risasi ya bega.”
Janette alionyesha jeraha la risasi na kuendelea kuzungumza jinsi
alivyosafiri mpaka kuingia Tanzania na misukosuko yote waliyokutana nayo
ambayo Mungu pekee ndiye aliyewaongoza lakini kwa uwezo wa kibinadamu
wangekufa.
“Ndugu zangu namalizia kwa kuwashukuru wote mliokuja hapa kunisikiliza
naomba taarifa zangu mzifikishe kwa watu wote ili wajue tofauti ya
Janette anayetafutwa na Melania msichana aliyeingia katika jeshi la
waasi baada ya ajali ya ndege. Mpaka hapa moyo wangu umekuwa mweupe kwa
vile nimetua mzigo uliokuwa moyoni mwangu kwa muda mrefu. Asanteni kwa
kunisikiliza na Mungu awabariki.”
Baada ya kusema vile alinyanyuka ili arudi hotelini, waandishi wa habari
walimzunguka kumuuliza maswali nini mstakabali wake baada ya kurudi
nyumbani.
Janette baada ya kufanikiwa kufika Tanzania ametoa yake ya moyoni yenye
kuumiza moyo mbele ya waandishi wa habari. Taarifa za safari yake kuja
Tanzania zilijulikana na vyombo vya dola vilikuwa vikimsubiri kwa udi na
uvumba. Baada ya kujitambulisha kuwa yeye ndiye anayetafutwa, serikali
ya Tanzania itachukua uamuzi gani? Kuyajua yote tukutane Hapa >>>INGIA HAPA
No comments:
Post a Comment