Stori: Shakoor Jongo na Musa Mateja
ZIKIWA zimepita wiki kadhaa tangu kuripotiwa kupatanishwa kwa mastaa
wawili katika tasnia ya filamu Bongo, Wema Sepetu na Kajala Masanja,
taarifa zisizo na shaka zilizotua kwenye meza ya Ijumaa Wikienda
zinaeleza kwamba upatanisho huo haukusaidia chochote na sasa bifu jipya
limeibuka kati yao.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha ndani kilichoomba hifadhi ya jina lake,
zoezi la upatanishi kati ya mastaa hao lililofanyika kwenye msiba wa
dairekta wa filamu za Kibongo, George Tyson, Mbezi Beach jijini Dar
lilikuwa sawa na kazi bure.
“Hakuna yeyote kati yao aliyekuwa na nia ya dhati ya kumaliza tofauti
zilizokuwepo, walikubali kupatana kwa sababu ya heshima ya waliokuwa
wanawapatanisha lakini kiukweli ilikuwa ni sawa na danganya toto, bifu
limelipuka upya,” kilisema chanzo hicho ambacho ni rafiki wa karibu wa
mastaa hao wakubwa mjini.
TEAM WEMA, TEAM KAJALA WANOGESHA BIFU
Kwa mujibu wa sosi wetu, ukiachilia mbali kukosekana kwa utayari wa
kupatanishwa kati ya wawili hao, pande mbili za mashabiki wao wenye
ushawishi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii waliojipachika majina ya
Team Wema na Team Kajala, zimekuwa zikinogesha bifu hilo kwa kumwagia
petroli kwenye moto, hali inayozidi kutibua mambo.
“Sikia nikwambie, kuna vitu vinafanyika katika mitandao ya kijamii hasa
Instagram kuhusiana na hizi pande mbili halafu wahusika wakuu
wanajifanya hawazijui, kuna Team Wema ambayo inamsapoti Wema na ile ya
Kajala inayoitwa Team Kajala, wenyewe wanawajua fika ni akina nani
wanaounda pande hizo ila ukiwauliza wanajifanya hawajui chochote.
“Wengine wananunuliwa mpaka simu za kisasa zenye uwezo wa kufungua
mitandao ya kijamii ili wasambaze uzushi na uongo kuhusu upande pinzani,
sasa timu hizo ziliposikia juu ya upatanisho huo, ziliwajia juu
wahusika ambapo kila mmoja kwa upande wake alikanusha kupatana na
mwenzake,” kilizidi kutiririka chanzo hicho.
KAJALA HATAKI KABISA SULUHU
Chanzo chetu kiliendelea kufunguka kuwa Kajala hataki kabisa kusikia
kuhusu mambo ya suluhu kwa sababu Team Wema imemdhalilisha sana
mtandaoni kiasi cha kumpa wakati mgumu kujieleza mbele ya mwanaye, Paula
ambaye inadaiwa naye aliyashuhudia matusi hayo ya nguoni.
“Yaani Kajala anasema labda Wema mwenyewe ndiyo aende kumuomba radhi kwa
kashfa zilizokuwa zinatolewa na timu yake anaweza kumfikiria mara
mbilimbili kuhusu suluhu na siyo kusuluhishwa juujuu tu kama
ilivyotokea,” alizidi kutiririka sosi wetu na kuongeza:
“We si unaona mara ngapi Wema na Kajala wanakutana sehemu na wewe
mwenyewe kama mwandishi unashuhudia, umewahi kuwaona wakiwa pamoja au
hata kusalimiana?”
MSIKIE KAJALA
Baada ya kusikia kauli hizo kutoka kwa chanzo chetu, kama kawaida ya
Ijumaa Wikienda liliingia mzigoni kutafuta mzani wa habari ambapo wa
kwanza kutafutwa alikuwa ni Kajala ambaye hakutaka kabisa kulizungumzia
kwa kina suala hilo. Hebu msikie:
“Kiukweli mi naona hili tatizo letu linachangiwa na hizi timu ambazo
zipo kwa ajili ya kuongeza matatizo. Nasikia eti baada ya siku ile mimi
na Wema kupatanishwa, watu wa timu yake walimpigia kumuuliza, akakataa
kuwa hajakubali kupatanishwa na mimi ili kuwafurahisha watu wake, sasa
unategemea mimi nitasema nini? Nafikiri siyo rahisi mimi kukaa karibu na
Wema kama zamani,” alisema Kajala.
WEMA NAYE
Kwa upande wa Wema yeye alishangaa habari hizo na kutoa dukuduku lake
kwa kusema anachojua ni kwamba hana bifu na mtu yeyote, siyo Kajala tu
bali mtu yeyote ambaye walikuwa na tofauti huko nyuma yeye hana bifu
naye tena.
“Mi nadhani watu wanahitaji kuona picha ambayo tumepiga pamoja na Kajala
ndiyo waamini kuwa tumemaliza bifu letu, unajua huu unaokuja ni Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan na mimi ni mtoto wa Kiislam sasa nitafungaje
Ramadhan huku nikiwa na bifu na mtu?” alisema Wema.
Kukinzana kwa maelezo ya wawili hao kunatosha kuonesha jinsi ambavyo suluhu ya awali haikuweza kumaliza bifu kati yao.
KUTOKA KWA MHARIRI
Wema na Kajala nyie ni wasanii wakubwa ambao jamii inawatazama kama kioo
chao. Haipendezi kuendeleza malumbano yasiyo na msingi, huu si wakati
wa kuwekeana visasi bali sameheaneni kutoka ndani ya mioyo yenu na
mshirikiane kuisimamisha sanaa ya filamu za Kibongo.
No comments:
Post a Comment