FACEBOOK

LightBlog

Breaking

LightBlog

Monday, 9 June 2014

Wabunge wawindwa


Mbunge wa Mbinga Magharibi, John KombaHOFU ya siasa za kuchafuana kuelekea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani imeanza kushika kasi miongoni mwa wabunge ambao tayari wameanza kuanikwa picha zao kwenye mitandao ya kijamii wakiwa faragha.
Tanzania Daima Jumapili, imedokezwa kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakifadhili upigaji wa picha za video na mnato kwa kuwatumia wahudumu wa hoteli mbalimbali za ndani na nje ya Mkoa wa Dodoma, kunakofanyika vikao vya Bunge.
Inaelezwa kuwa lengo la kufadhili mikakati hiyo ni kuwaharibia majina wabunge husika ili wasipate fursa ya kuaminika kwenye jamii, hivyo kunyimwa kura katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu mwakani.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano, baadhi ya wataalamu wa masuala ya mitandao wamekuwa wakitengeneza picha za ngono kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.
Inadaiwa baadhi ya watu huwasiliana na wahusika juu ya picha hizo huku wakiwatishia kuwa endapo wasipowapa fedha watazitoa kwenye jamii.
Tayari picha za Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba (CCM) na Ukerewe, Salvatory Macheli (CHADEMA), zimetolewa zikiwaonyesha wakiwa faragha.
Komba, alikaririwa na vyombo vya habari kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia teknolojia kutengeneza picha hizo kwa malengo ya uovu.
Wabunge wanena
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili, baadhi ya wabunge walilaani picha hizo kuwekwa kwenye mitandao na kutaka zitungwe sheria kali kuwadhibiti watu wanaozisambaza au kuzitengeneza.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema picha zilizoonyeshwa kwenye mitandao hazifai kushangiliwa na wabunge kwakuwa hawajui kesho au siku zijazo za nani zitatolewa.
Alisema picha za aina hiyo mbali ya kuwachafulia majina wabunge kisiasa, lakini pia zina athari kwa famililia na jamii inayowazunguka wahusika.
Lugola, alisema picha hizo zinaonyesha kuwa zimepigwa hotelini, hivyo kuanzia sasa wabunge watakuwa waoga kwenye kutafuta malazi wakiwa ndani au nje ya Dodoma.
“Picha hizo kama ni za kweli kuna mambo mawili makubwa… kwanza inawezekana wafanyakazi wa hoteli au wahudumu ndio wanaozipiga hizo picha kwa kutumiwa na makundi ya wanasiasa, kama ni hivyo wabunge wote hawako salama, hivyo ni suala linalohitaji mjadala wa kulikemea,” alisema.
Alisema kama ni za kutengeneza, jambo hilo linapaswa kulaaniwa kwa watu kutumia teknolojia vibaya kuchafua wenzao.
“Ni kinyume cha katiba kwa mtu kuingilia mambo ya mtu binafsi, wanaoziweka kwenye mitandao wanavunja sheria, wachukuliwe hatua kali,” alisema.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (CHADEMA), alisema amesikitishwa na kitendo hicho cha kuweka mambo binafsi kwenye mitandao kwakuwa  wabunge wameapa kuilinda katiba siyo kwenda kuzungumzia masuala binafsi kama yaliyosambazwa kwenye mitandao.
Alisema hivi sasa kumekuwa na kasi ya kusambazwa kwa picha hizo, hasa zikiwagusa wanasiasa, wasanii, wafanyabiashara na watu wenye hadhi katika jamii kwa lengo la kuwakosanisha au kujitafutia fedha.
Wenje alisema kutokana na ongezeko la vitendo hivyo, tayari ameandika muswada atakaouwasilisha kama hoja binafsi kutaka itungwe sheria kali kwa watu wanaosambaza picha za utupu na muswada wa kupinga ushoga.
“Nalaani kitendo hicho, sijui kama hoteli tuliyopigwa ni Dodoma au la, yanaweza kuvunja nyumba, kupotea kwa amani katika siasa, ndoa, jamii na kwingineko. Nashauri zitungwe sheria kali haraka kuwadhibiti wasambazaji wa picha hizo mitandaioni,” alisema.
Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), alisema analaani usambazaji wa picha hizo na jamii haipaswi kuzoea hali hiyo kwa kuwa ni kinyume na maadili ya Kitanzania.
“Wabunge waliopigwa picha zile zikiwa halisi wamelifedhehesha sana Bunge ingawa ni masuala binafsi, kama ni za kutengenezwa… wanaozitengeneza na kuziweka kule kwa lengo la kuwachafua wanasiasa wachukuliwe hatua kali kwa kuwa wanakiuka katiba ya nchi,” alisema.
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), alisema kuwekwa kwa picha hizo ni propaganda na mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya wanasiasa katika mitandao.
“Hizo ni siasa za maji taka… lakini ni changamoto kwa viongozi kama kweli wana nyendo ambazo haziko sawa kwa kuwa ni aibu kwa taifa na wananchi wanaowaongoza kama picha hizo zitakuwa na ukweli,” alisema Mdee.
Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (CHADEMA), alisema picha zote zilizotolewa ni za uongo, hakuna ukweli wowote kuhusu matukio hayo na hao waheshimiwa.
“Ujinga huu unaofanywa na mitandao ya kijamii wenzetu Ulaya hawafanyi hivyo, bali wanaweka masuala ya msingi yenye ukweli… hayo ni mambo ya kitoto,” alisema Lyimo.
Lyimo alisema hata kama kuna uhuru wa habari, ni vyema wenye mitandao wakafuata maadili ya habari na picha zipi zinapaswa kutolewa na siyo kutoa kila kitu, isitoshe cha uongo.
“Hawa waheshimiwa waliotolewa picha za ngono na hii ya mwenyekiti wangu akiwa na shati la CCM… ambayo inawekwa mara kwa mara, wajue kwamba hawa ni watu maarufu wenye wananchi wanaowawakilisha na familia zao.
“Nawashauri wenye mitandao ya kijamii kutumia maadili ya uandishi wa habari vizuri na siyo kutupia kila kitu mtandaoni, tena matukio ya kupotoshaji,” alisema.
TCRA wanena
Meneja Huduma za Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungi, alisema ni kosa la jinai kusambaza picha chafu kwenye mitandao ya kijamii.
Mungi, alibainisha kuwa TCRA wanapinga utaratibu huo na walianzisha kampeni  ya ‘Futa  na Delete Kabisa’ iliyozinduliwa mwaka jana inayowahamisha na kuwaelimisha Watanzania kufuta ujumbe au picha yoyote isiyofaa katika simu au mitandao ya kijamii.
Alisema  Watanzania wanatakiwa kuacha ushamba wa kutumia mitandao ya  kijamii vibaya badala yake waitumie katika kuleta maendeleo.
“Kuweka na kusambaza picha za utupu au zozote chafu katika mitandao ni kosa la jinai, lakini pia Watanzania wanapaswa kutambua kuwa  TCRA haina mamalaka ya kusimamia makosa ya jinai isipokuwa ni polisi pekee,” alisisitiza.

No comments:

Adbox