MSANII Emmanuel Mbasha (32) na mume wa Mwimbaji wa Injili, Flora Mbasha,
amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na mashitaka
mawili likiwemo la ubakaji.
Mshtakiwa huyo ambaye ni mfanyabiashara na mwimbaji alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Wilberforce Luago.
Wakili wa Serikali Nassoro Katuga alidai kuwa mshtakiwa alitenda makosa
hayo mawili maeneo ya Tabata Kimanga, jijini Dar es Salaam.
Katuga alidai katika shitaka la kwanza kuwa, Mei 23, mwaka huu eneo la
Tabata Kimanga, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, kinyume cha
sheria huku akijua ni kosa alimuingilia kwa nguvu msichana anayedaiwa
kuwa shemeji yake (jina limehifadhiwa).
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mei 25, mwaka huu eneo la Tabata
Kimanga, jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria, mshtakiwa
alimuingilia kwa nguvu mfanyakazi wake (jina limehifadhiwa).
Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashitaka hayo .Upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi la dhamana.
Hakimu Luago alitaja masharti ya dhamana kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini
wawili, mmoja awe mtumishi wa serikali na mwingine kutoka taasisi
inayotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 5.
Mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo alipelekwa
rumande na kesi iliahirishwa hadi Juni 19, mwaka huu itakapotajwa.
Mbasha akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi alisindikizwa katika basi
la Jeshi la Magereza kwa ajili ya kwenda kuanza maisha mapya mahabusu ya
Keko, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment