SIKU moja baada ya Naibu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Mwigulu Nchemba
kunukuliwa na gazeti la serikali la Habari Leo akitamba kupinga nyongeza
ya siku 60 za Bunge la Katiba, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa
chama hicho, Nape Nnauye, amempinga akisema hawezi.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alitoa tambo hizo juzi
mjini Iringa wakati akihutubia mkutano wa hadhara, akisema kuwa atapinga
kwa nguvu zake zote Bunge hilo kukutana kwa siku nyingine 60.
Hata hivyo, msimamo wake unakinzana na chama chake ambacho kimeapa
kwamba hata kama wajumbe wenzao wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
wasiporudi bungeni, wao wataendelea na Bunge hadi katiba mpya ipatikane.
Katika kikao chake cha Kamati Kuu cha hivi karibuni, CCM iliazimia
kupambana na UKAWA popote, nje na ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, huku
ikisisitiza kwamba haiwezi kuwabembeleza warudi bungeni kwa sababu
chama hicho kinao wajumbe wa kutosha kutimiza theluthi mbili ya kura
zinazotakiwa kikanuni.
Kufuatia mkorogano huo, Tanzania Daima Jumatano lilimtafuta Nape jana kwa simu akiwa ziarani mkoani Manyara ili kupata msimamo wa chama kuhusu katiba mpya.
Katika majibu yake kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu, Nape alisema:
“Gazeti la Habari Leo limemnukuu vibaya Mwigulu. Hawezi kupinga jambo ambalo rais amelipitisha.
“Chama kupitia vikao halali kimeishatoa tamko na msimamo unajulikana.
Vinginevyo ili ampinge rais, yeye kama naibu waziri alipaswa ajiuzulu
kwanza. Hata hivyo, naibu waziri haruhusiwi kuwasilisha hoja binafsi.”
Kwa mkanganyiko huo, ni dhahiri CCM wanakinzana katika suala zima la
upatikanaji wa katiba mpya inayotokana na matakwa ya wananchi.
Itakumbukwa kuwa katika siku za hivi karibuni kwenye mikutano yao ya hadhara iliyofanyika visiwani Zanzibar
na mkoani Tabora, CCM kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana
na Nape walisema kuwa hawahitaji katiba mpya kwa sababu sio muarobaini
wa matatizo waliyonayo wananchi.
Viongozi hao walisisitiza kuwa hata katiba mpya ikipatikana itawekwa
kabatini, huku Nape akizidi kuwashambulia wajumbe wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, akisema wamekengeuka kwa mapendekezo yao ya muundo wa serikali tatu.
Licha ya rasimu ya katiba kupendekeza muundo wa serikali tatu, CCM
imekuwa ikiendesha harakati za kuipindua, ikitetea muundo wa sasa wa
serikali mbili uendelee, jambo linalopingwa na UKAWA hadi kufikia hatua
ya kutoka nje ya Bunge hilo.
Katika mkutano wake wa mjini Iringa, Mwigulu alipinga Bunge hilo
lisiongezewe muda kwa madai kwamba likiendelea kwa mtindo kama wa awamu
ya kwanza, itakuwa sawa na kutumia vibaya fedha ya walipa kodi.
Aliahidi kumshauri Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, amuandikie
barua Rais Jakaya Kikwete, ili avunje Bunge hilo endapo wajumbe wake
watashindwa kutumia wiki mbili za mwanzo kujadili mambo ya msingi katika
rasimu hiyo.



No comments:
Post a Comment